Okoa Mombasa inapongeza notisi iliyochapishwa na Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) hivi leo, ambayo ikitekelezwa ipasavyo, inafaa kurudisha huduma kamili za bandari Mombasa baada ya kutokuwepo kwa miaka zaidi ya mitatu.
Notisi ya KPA inasema kwamba waagizaji bidhaa sasa wanaweza kuchagua mahali au vituo vya makasha wanaopendelea na njia ya kusafirisha mizigo. Tangu 2019, maagizo ya serikali yamewataka waagizaji kusafirisha mizigo ya kuelekea bara kupitia Reli ya Standard Gauge (SGR) na kupokea mizigo yao kwa vituo vya KPA mjini Nairobi au Naivasha. Tunatafsiri notisi hii kumaanisha kuwa ukiritimba uliopewa SGR wa kusafirisha makasha umefutiliwa mbali, kama alivyo agiza Rais Ruto baada ya kuapishwa kwake.
Tunapongeza hatua hii kwa sababu ukiritimba wa SGR dhidi ya uchukuzi wa shehena umeharibu uchumi wa bandari ya Mombasa katika muda wa miaka mitatu iliyopita. Maelfu ya wamiliki wa malori na madereva walipoteza riziki zao; makampuni zinazotoa huduma na nyaraka za utoaji wa mizigo walihamia bara na zengine kufungwa; Vituo vya makasha havikuwa na maana na maelfu ya watu wanaofanya kazi katika sehemu za wauzaji wa malori, vituo vya kuuza mafuta, makanika, wafanyabiashara wa vipuri, mikahawa vibanda vya sekta isiyo rasmi, uchuuzi, waliachwa bila kazi.
Ilani ya leo inamaanisha kuwa uchumi wa Mombasa utafufuka na kufanya kazi tena, na jiji letu litajengeka tena. Haitafanyika kwa haraka lakini tuna imani kwamba ari ya wakazi wa Mombasa, bidii na werevu vitarejesha jiji letu katika umashuhuri wake wa zamani.
Pia tunatumai notisi hii itaashiria mwisho wa sera ya serikali ya kulazimisha Mombasa kubeba sehemu kubwa ya mzigo wa KES 450 bilioni (USD 4.2 bilioni) katika mikopo iliyochukuliwa na serikali kujenga SGR. Sera hiyo kimsingi ilitoa dhabihu uchumi wa Mombasa katika jaribio la kulipia mradi uliobuniwa vibaya na wa bei ya juu.
Kwenda mbele, Okoa Mombasa itaendelea kutekeleza lengo lake la kuhakikisha ushirikishwaji wa umma katika maamuzi yote yanayohusu rasilimali za ndani. Pia tutakuwa macho katika kufuatilia utekelezaji wa notisi ya KPA ya leo, ili kuhakikisha kuwa waagizaji wa mizigo wanapewa uhuru wanaostahili.
Hatimaye, Okoa Mombasa anatoa wito kwa Serikali kutupilia mbali rufaa yake ya uamuzi katika Malalamiko ya Kikatiba Na. 159 ya 2018 na Na. 201 ya 2019 (Rufaa ya Kiraia Na. E.12 ya 2021). Katika kesi hiyo, Mahakama Kuu iligundua kuwa maagizo ya shehena ya SGR yalikuwa kinyume na katiba. Huku maagizo hayo yakibatilishwa, kesi hiyo sasa imekwama. Serikali iondoe rufaa yake mara moja.
Pia tunatoa wito kwa Rais Ruto kutii agizo la mahakama ambalo halijakamilika la kutaka serikali itoe hadharani kandarasi na makubaliano yote yanayohusiana na mipango, ujenzi na utendakazi wa SGR. Wanachama wa Okoa Mombasa walishinda agizo hilo la mahakama mwaka wa 2021, lakini rufaa ya serikali bado inasubiri.